A joint initiative by the United Nations, The Government of Tanzania and The Economic and Social Research Foundation  

Mkakati Mrithi – MKUKUTA II: Je, ni Mkakati Sahihi?

Tanzania Bara ilianza utekelezaji wa awamu ya pili ya Mkakati wa Kupunguza Umasikini mwaka 2005/06. Mkakati huo ulitokana na mapendekezo ya mapitio ya awamu ya kwanza ya Mkakati wa Kupunguza Umasikini (PRSP). Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Tanzania (MKUKUTA) umekuwa ndiyo mfumo wa kitaifa wa kuelekeza namna ya kuleta maendeleo na kuondoa umasikini Tanzania (Bara) kwa kipindi cha miaka mitano. MKUKUTA I unamalizika mwezi Julai 2010. Baada ya hapo, Serikali imeandaa Mkakati Mrithi (MKUKUTA II) kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Kwa utaratibu shirikishi na mashauriano mapana zaidi, rasimu ya Mkakati Mrithi (MKUKUTA II) imeshasambazwa kwa wadau kwa ajili ya majadiliano.

Wakati wa mapitio ya MKUKUTA I, mambo mbalimbali yanayohusu utekelezaji katika kipindi chote cha utekelezaji wa mkakati huo yalizingatiwa. Miongoni mwa hayo ni:

Kutokuwepo vipaumbele vya kutosha na uratibu wa utelekelezaji wa mkakati: Ijapokuwa kwa juhudi za makusudi upangaji vipaumbele ungeliweza kufanyika katika ngazi ya kisekta na makundi, hili halikufanyika vya kutosha kwa sababu ya ukosefu wa miongozo ya kutosha (k.v sekta mbalimbali hazikwenda sambamba na MKUKUTA). Uratibu haukuwa wa kuridhisha (k.f uratibu wa mfuatano wa vifungu vya MTEFs vya MDA mbalimbali katika kuchangia matokeo fulani ulikuwa dhaifu.)

MKUKUTA kutokuwa na fedha za kutosha: Kuupatia fedha MKUKUTA kulihitaji iwepo mipango ya uwekezaji ambayo ingeliingiza fedha za kughalimia shughuli za maendeleo. Kwa mkakati unaomalizika, hili halikuwezekana kwa sababu upangaji wa gharama halisi (costing) za utekelezaji wa mkakati ulikawia kufanyika.

Uwezo mdogo wa kugharamia MKUKUTA: Kugharamia MKUKUTA kulihitaji ubunifu wa mipango ya uwekezeji ili kupata fedha ya utekelezaji. Hili halikufanyika na tafiti za kung’amua gharama halisi za kiutekelezaji zilichelewa kufanyika

Kutokuwepo maelekezo ya kutosha juu ya namna ya kusaidia utekelezaji wa MKUKUTA: MKUKUTA ilibidi usaidiwe na mikakati na sera nyingine katika utekelezaji wake. Sera na mikakati mingi iliopo hivi sasa havikwenda sambamba na MKUKUTA, mara nyingine baadhi ya sera na mikakati ilikinzana na MKUKUTA.

Utaratibu dhaifu wa Kufuatilia na Kufanya tathmini: Mfumo wa kitaifa wa ufuatiliaji umaskini (PMS) ulikuwa dhaifu kwa sababu haukuzifikia jamii nyingi za kitanzania. Kwa hiyo, wengi miongoni mwa wale waliotarajiwa kunufaika na MKUKUTA walikuwa hawaelewi juu ya utekelezaji wa MKUKUTA I.

Kutokana na udhaifu uliokuwa wazi wa MKUKUTA I, Mkakati Mrithi umeongezewa yafuatayo:

Uratibu madhubuti kwa upatikanaji wa matokeo: Mkakati mpya utaendeleza mafanikio ya mkakati unaomalizika na kushughulika upungufu wake kwa kutoa miongozo ya kutosha juu ya uwekaji wa vipaumbele na kuimarisha uhusiano na asasi toka katika sekta mbalimbali.

Kulenga vizuri maeneo ya kuyashughulikia: Mkakati huu utayalenga maeneo ya kushughulikiwa vizuri zaidi, pia utayaelezea matokeo yanayotarajiwa na jinsi ya kufikia matokeo hayo. Mkakati huu utachagua matokeo muhimu machache yakupewa kipaumbele kama vile shughuli za kiuchumi za kilimo na zisizokuwa za kilimo, miundombinu, elimu bora na upatikanaji sawa wa elimu, afya bora, maji na udhibiti wa maji taka na kuimarisha utawala bora na uwajibikaji.
Rasimu ya MKUKUTA II inapatikana katika tovuti ifuatayo:

http://www.tzonline.org/pdf/mkukutalldraft.pdf

Majadiliano haya yanakusudia kuonesha kiwango ambacho Mkakati Mrithi ulivyotilia maanani upungufu wa MKUKUTA 1. Zaidi ya hilo majadiliano haya yamedhamiria kutathmini uwezo wa MKUKUTA II katika kuyafikia matokeo yaliyoainishwa, malengo yaliyokusudiwa pamoja na Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs). Kwa hivyo, majadiliano yetu yalenge katika kuyajadili masuala yafuatayo:

• Je! MKUKUTA II ni tofauti na MKUKUTA I? Kwa vipi?
• Ni mambo gani yaliyopelekea kutofikiwa kwa baadhi ya malengo ya MKUKUTA I?
• Je! MKUKUTA II umejumuisha kila kitu na ni madhubuti vya kutosha kuyafikia matokea na malengo yote yaliyoainishwa?
• Lipi la ziada linalohitaji kutekelezwa?

Home