A joint initiative by the United Nations, The Government of Tanzania and The Economic and Social Research Foundation
Topic : Vifo Vya Akina Mama Kutokana Na Matatizo Ya Ujauzito(Maternal Mortality) ni tatzo kubwa Tanzania : Nini kifanyike kutatua tatizo hili?*
Mbali na jitihada za dhati zinazofanywa na serikali yetu kwa muda mrefu kutatua tatizo la vifo vya akina mama kutokana na matatizo ya ujauzito (martenal mortality), takwimu za karibuni zinaonyesha hali sio nzuri kwani vifo vya akina mama vinaendelea kuongezeka kila mwaka. Bila ya mi
...Click here to read more
Mbali na jitihada za dhati zinazofanywa na serikali yetu kwa muda mrefu kutatua tatizo la vifo vya akina mama kutokana na matatizo ya ujauzito (martenal mortality), takwimu za karibuni zinaonyesha hali sio nzuri kwani vifo vya akina mama vinaendelea kuongezeka kila mwaka. Bila ya mikakati thabiti kuelekezwa katika kutatua vyanzo vya tatizo hili kuna uwezekano wa kuendelea kuwapoteza; mama zetu, dada zetu, shangazi zetu na hata mabinti zetu kila siku. Hakika kila mtu anaguswa na vifo hivi, hivyo basi hatuna budi kushiriki katika kupeana mawazo ya jinsi ya kutatua tatizo hili.
Je vifo vya akina mama kutokana na matatizo ya ujauzito ni tatizo nchini? Ndiyo! Ni tatizo, tena ni tatizo kubwa sana, na hasa ukizingatia kwamba tatizo hili limekuwa sugu kwa muda mrefu hapa nchini Tanzania. Bado miaka mitano tu kufikia mwaka 2015, mwaka ambao malengo ya maendeleo ya millennia (MDGs) yamepangwa kufikiwa,Kuna matumaini madogo sana kwamba serikali ya Tanzania itaweza kufikia lengo la 5 (MDG 5) – kupunguza vifo vya akina mama kutokana na matatizo ya ujauzito kwa asilimia sabini na tano kati ya mwaka 1990 na 2015.
Takwimu za sensa ya afya za mwaka 2004 (TDHS 2004) zinaonyesha vifo vya akina mama kutokana na matatizo ya ujauzito vimezidi kuongezeka nchini Tanzania, kutoka vifo 529 kati ya akina mama 100,000 wanaojifungua katika mwaka 1996 mpaka kufikia vifo vya akina mama 578 kati ya akina mama 100,000 wanaojifungua katika mwaka 2004. Hivyo inaonyesha basi pamoja na jitihada zote za serikali kuondoa tatizo hili bado linaendelea kuongezeka siku hadi siku na hivyo tunazidi kupoteza maisha ya wapendwa wetu!. Na zaidi ya hili ni muhimu kujua kwamba zaidi ya akina mama 250,000 wanapata vilema vya kudumu kila mwaka kutokana na matatizo ya uzazi .Idadi hii ni kubwa, inatisha na inahitaji dhamira ya dhati kuondokana na tatizo hili.
Kuna jitihada zozote za kutatua sababu za vifo hivi? Ndiyo!Baadhi ya jitihada zinazofanywa na serikali ni kama kuongeza vyuo vya udaktari, wauguzi n.k ili kutatua tatizo la upungufu wa watoa huduma, Serikali imejitahidi pia kupeleka madawa na vifaa vya tiba kufikia ngazi ya zahanati ili kupunguza uhaba huo, pia imepitisha sheria ya kuruhusu huduma za ujauzito na huduma za rufaa (gari la wagonjwa) kutolewa bure ili wajawazito wengi wapate huduma salama, na inaendelea na mchakato wa kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa jamii kupitia wizara yake ya afya.
Maeneo ambayo bado yanaleta utata na kuhitaji ufumbuzi wa haraka? 1. Mbali ya jitihada zote zinazofanywa na serikali, watu binafsi na vyama vya kiraia vifo vinaendelea kuongezeka, nini hasa ni sababu ya tatizo hili? nini cha zaidi kifanyike? 2. Ni muhimu kujua kwamba ni asilimia 46% tu ya akina mama Tanzania wanajifungulia kwenye vituo vya afya? Tutaibadilisha vipi hali hii? 3. Mbali na sheria ya huduma za kujifungua ( pamoja na huduma za rufaa) kutakiwa kutolewa bure katika vituo ya afya vya serikali, bado hali inaendelea kuwa mbaya , tatizo ni nini? nini kifanyike zaidi? 4. Iko wapi nafasi, na kikomo cha wakunga wa jadi katika mfumo mzima wa utoaji huduma kwa mama wajawazito? Je unafikiri washirikiane vipi na wizara husika?
*Dr Riziki Ponsiano: HPV-vaccine project coordinator(MD, PGD-Mch, MPH-Social & Behvrl science) and Dr Tausi Kida ( PhD Dev Economics) ; Project Coordinator; ESRF/REPOA/ISS Capacity Building - Poverty Analysis
Wengi wa wachangiaji wamechangia kwa usahihi kabisa. Labda niongezee. Tatizo kubwa la Tanzania na pengine la nchi nyingi za Afrika, ni lile ambalo alishawahi kuliandika kwa kirefu, mwandishi wa habari maarufu hapa nchini. Tatizo letu ni Uongozi, uongozi, uongozi. Basi!
Viongozi wetu hawajatoa kabisa nafasi katika kuwekeza kwenye huduma ya afya. Wanachojua wao ni kuwepo kwa zahanati pekee katika kijiji X bila kujali kama kuna wahudumu wa afya au la.
Tembeleeni katika zahanati za vijiji vyetu. Utakuta jengo na mhudumu wa afya mmoja (Medical Attendant). Ukibahatika sana, utamkuta ameongezeka Tabibu mmoja tu. Sasa, kwa mazingira haya utategeaje huduma bora?
Mimi ningeishauri serikali yetu iwekeze katika huduma za afya na vifo vya wajawazito vitakuwa historia.
Frank
Marjorie Mbilinyi : Friday, September 03, 2010
Pamoja na kukubali kwamba kuna ukandamizaji hali ya juu kwa wanawake wakati wa kujifungua, ni muhimu kuchunguza zaidi sebabu kiini .. kuanza na mfumo wa sekta ya afya, nafasi ya wanawake wakiwa wafanya kazi au wateja/clients .. na jinsi wahudumu wanawake wanavyo kandamizwa na kunyonywa na mfumo mwenyewe .. pamoja na wafanyakazi wote hasa katika ngazi ya chini -- wanaotoa huduma za kila siku ikiwa usafi pamoja na zote nyingine muhimu
ukimwona mnyonge anamkandamiza mnyonge mwenzake muhimu kuuliza kwanza kwa nini anafanya hivyo badala ya kutambua adui yake ni nani? Kwa kila hadithi mbaya juu ya uzoefu wa uzazi, bila shaka kuna hadithi nyingine nzuri juu ya wahudumu waliosaidia kuokoa maisha ya mama na/au mtoto .. na wakati huu serikali yetu inakataa kuelekeza pesa zinazotakiwa kwa huduma za afya, na kuhakikisha kwamba pesa zinafika na kunufaisha mgonjwa pamoja na mhudumu wa afya mwenyewe -- na si mikutano, safari za nje, na kadhalika
kama wengine wengi waliotangulia wamekwisha kusema, kiini cha vifo vya akina mama wakati wa mja mzito ni kutokuwa na wahudumu wa kutosha na wenye mafunzo/ staadi inayotakiwa; umbali wa vituo vya afya kwa wanawake; gharama za safiri; gharama za huduma kinyuma cha sheria; kutokuwa na vituo vya kutosha vyenye huduma za emergency obstetricic [sp?] care .. ki msingi wake serikali yetu haijaweka kipaumbele kwa huduma za afya na hasa afya ya uzazi -- na si serikali tu, hata wanasiasa, hata waBunge, na hasa sisi raia hatujadai uboreshaji wa huduma za afya ya uzazi na kudai haki ya wanawake kuzaa bila hatari ya vifo ..
kilwa mwaka wanaharakati wanaongea juu ya idadi ya wanawake wanaokufa katika uzazi zaidi ya wanawake 25 KILA SIKU .. je waangapi tumeshangaa na kuandika barua kwa wahusika au gazeti? waangapi tumedai ilani ya uchaguzi ya kila chama ieleze mkakati gani kuboresha huduma za afya? au kufanya maandamano?
wape wahudumu wa afya motisha na nyenzo za kufanya kazi zao na heshima inayostahili na watatoa huduma nzuri. Suala ni mfumo, sera na bajeti .. na kimsingi ya yote ni jamii yetu ambayo haithamini ya kutosha maisha ya mwanamke.
Marge
costa john kanaysu : Friday, September 03, 2010
Tanzania kama nchi zingine masikini dunian bado ina mambo mengi ya kufanya, lipo la afya,shule na mawasiliano.Tumejikuta katikati ya uhitaji wa mahitaji haya kwa pamoja bila kujali lipi ni bora kuliko jingine na issue hapa siyo matajili kuumiza masikini hapana ni mabadiliko katika kuishi yanayoikabili dunia nzima.
zamani tulizoea sana kupewa huduma bure wengi hawajui sababu,wakati huo nchi yetu kama zilivyokuwa nchi zingine africa hasa za kijamaa zilikuwa zinafaidika na ugonvi baridi kati ya magharibi na mashariki na ili hawa wakubwa wapate wakuwaunga mkono walijipendekeza kwetu, leo haiwezekani.
nini kifanyike sasa? ni vyema watanzania tukabadilika kutoka huko tulikokuwa kuja kwenye karne hii,kama unajua mkeo amekalibia kujifungua weka hakiba na uanze kujua ni wapi mkeo atajifungulia, kama fedha huna sogea kalibu na hospitali za serikali.
pili tuelewe fika kwanza mimba siyo heart attack kwamba inakuja ghafra,unapoamua kuzaa lazima ujue kuna gharama inakuwaje upate hela ya mahali au ya chumba kama ni starehe alafu ukose elfu tano ya faili hospitali tujifunze kuweka akiba sasa hata huko kwenye kata na vijiji dispensary zipo na serikali imetoa vibari kwa wataalamu kuanzisha vituo na dispensary watu hawaendi wanasubiri wakatibiwe bule mambo haya yamepitwa na wakati hakuna dunia leo ambapo watu wanalala kungoja kupata huduma bule eti kwa kuwa kuna matajili wakubwa au kuna serikali italeta no no no no no no no no no!
TEL 0282540050-OFFICE 0732/0767/0715/0784643322 MWANZA-TANZANIA.
japjet Makongo : Friday, September 03, 2010
Sina uhakika kama nitakuwa narudia yaliyosemwa na wengine.
Kimsingi, sababu za ongezeko la vifo gvya akina mama wajawazito zimejika katika umaskini zaidi. Tafiti zinatuonyesha kuwa vifo vingi vinatokea kwa familia maskini na zilizo mbali na huduma. Hivyo ni busara kulichukulia tatioz hili katika awamu tatu..... za muda mfupi, kuhakikisha walio na tatizo kwa wakati huo wanapata huduma bora...pengine hapa ndipo ahadi ya mheshimiwa mgombea kura (mgombania kula) ya kutoa bajaji zinaweza kusaidia, japo kuna uwezekano wa baadhi kushindwa gharama. Pia bajaji hafiki kila mahali..sehemu za milima na visiwa vidogo Ukerewe, na Kilwa!
Pili ni mikakati ya muda wa kati, kutoa elimu ya uzazi, na kuboresha huduma katika vituo na majumbani, na tatu ni suala al muda mrefu kuhakikisha kuwa kuna mikakati ya dhati ya kusadia jamii kuongeza kipato chao. Haiwezekani wakina mama toka Lushoto na sehemu zinazotoa matunda kwa wingi wafe wakati matunda yao poia yanaoza bila soko! TUNAHITAJI DHAMIRA YA KISIASA.
MAKONGO
S. Moyo : Thursday, September 02, 2010
Poleni akina mama kwa kunyanyaswa na wanawake wenzenu. Naamini adui wa mwanamke ni mwanamke mwenyewe.
Hii ni kwa sababu vifo vingi vya akina mama havitokani na matatizo makubwa ya kisayansi ya kitabibu ila usimamizi mbovu, roho mbaya , rushwa na kutojali kwa manesi wetu. Hivi vitimbi ndivyo vilivyopo mahospitalini. Imagine umempeleka mama mjamzito hospitali unaambiwa hutapewa huduma mpaka ukamilishe pesa uliyodaiwa kwa rushwa.
Nenda kasikilize matusi manesi wanavyo tukana wajawazito. Mama akiomba msaada utasikia mfuate huyo aliye kupatia mimba. Mara usitusumbue hatupo kwa ajili yako hapa mara unataka nijigawe ili nimhudumie huyu na wewe nikuhudumie. Nimepate kumsikia nesi akisema kuwa huyu mwanamke asije akatulaza macho. Sisi tumechoka, muache sisi twende tukalale kule tumechoshwa na kelele zake.
Je yote haya yanahitaji mtaalamu. Je hujashuhudia nesi kamsusia mama mjamzito eti tu kwavile hakufuata maelekezo ya nesi labda kwa vile maumivu yamemzuia huyu mama asitende kama alivyoelekezwa. Kuna mengi tu na ya kutisha zaidi. Nimeshuhudia mama mjamzito kaachwa mapokezi mpaka kafariki bila hata kuhudumiwa. Ndugu za dada huyu waliambiwa bila alfu 75 mgonjwa wenu hapati huduma kwa dactari. Wakinamama hawa wakiendelea kuchangishana mmoja hadi mwingine wakimfuata huku hadi kule huko morogoro, mwishowe baada ya masaa karibu nane baada ya pesa kutopatiokana akafariki. Huyu alikuwa muhudumu wa Bar.
Hii ni aibu na inatisha sana kupeleka mjamzito katika hospitalizetu. Na hivi vyote havihitaji utaalamu wa kiwango cha juu. Kwa ukarimu tu, kupunguza rushwa, kutoa huduma ya haraka na kumjali mgonjwa na matakwa yake, vifo vitapungua kwa aslimia 90. Nenda Fast Track muhimbili uone hali ilivyo. Ndipo utagundua kuwa hatuna haja ya kuajiri dactari bingwa maana huku kote hatujafika. Nadhani kunahaja ya kuongeza huduma ya wakunga wa jadi maana hawa huduma yao ni muhimu mno. Wanaupendo na mara kwa mara wamezalisha wajawazito pale manesi wanapo wakataa au kuwa temndea ukatili.
Wanaume wanatakiwa sasa waichukue kazi hiyo maana akina mama hawaoneani huruma. Ndo maana panapo kuwa na mkunga mwanamme akina mama wanamkimbilia na kumganda kama luba.
Dr salatiel Moyo Simon Mwakyambiki
nyangubho nyega : Wednesday, September 01, 2010
Tunakushukuru muheshimiwa Bariki Kaale.
Mchango wako ni mzuri sana, binafsi ningependa uingie deep zaidi kutuonyesha ni kwa vipi sasa hizo data na tafiti mbalimbali zitasaidia kutafiti na kupunguza vifo vya akina mama na matatizo ya ujauzito, hasa ukizingatia wakati huu ambapo wagombea wetu wanatoa ahadi tele. Mfano mgombea wa ccm ameahidi kupelekea akina mama wajawazito bajaji 400! What is the relationship with Maternal martality? au bora liende!
Naomba mchango wako tena baada ya kupata detailed data za deforestation rate,nguvu za nishati hakuna, are the bajaji a soln for reducing maternal mortality? We need to think twice if this is from national perspective! What should be short/long strategic planning? apart from tree planting and eviction of cattle grazers from water sources.
senorina kimario : Wednesday, September 01, 2010
Chanzo cha tatizo hilo ni umaskini na ubinafsi kwa watu wachache wenye navyo wanotumia rasilimali za nchi kwa manufaa yao wenyewe.mfano mzuri ni maeneo ya vijijini barabara mbovu , huduma ya usafiri hamna na watu wanatumia baiskeli kuwapeleka wajawazito kwenye vituo vya afya jambo linalohatarisha maisha yao.mama anapotaka kujifungua mpaka afike kwenye kituo cha afya .inakuwa tabu ndio maana wengine wanajifungulia majumbani na barabarani wakiwa kwenye process za kwenda hospitali
Maoni yangu ni kwamba serikali ni lazima ijenge vituo vya afya huko vijijini ili wajawazito wapate huduma inayowastaili na pia kuwa na madaktari na wauguzi wa kutosha sio wanganganie mijini.pia miundo mbinu kama barabara ni lazima serikali iweke mpango wa kuziboresha ili ziweke kupitika kwa kipindi chote cha mwaka.Serikali ni lazima iipe sekta ya afya kipaumbele na wauguzi wawe naukaribu na wagonjwa wote bila kujali wala kuangalia vipato vyao ili waweze kutimiza majukumu yao ya kulinda afya ya kila mtanzania.
Marja-Liisa Swantz : Wednesday, September 01, 2010
Kwa Martin Mandalu na wanaume wengine. Wasichana wa umri chini ya miaka 15 hata wasichana wakubwa zaidi hawapati mimba kama hawakaribiwi kwanza na wanaume na kuwavuta kwa tendo hili. Ninyi wanaume mzungumze jinsi ya kubadilisha vitendo na tamaa za wanaume. Mtwara ngoma za wasichana za unyago zinachezwa umri mdogo mno. Kwa kufuata mila waliweza kuanza kucumbiana baada ya unyago. Siku hizi ngoma hizi hazina maana. Bibi Marja Swantz
Godliving J. Kessy : Thursday, August 05, 2010
Brethren good day!
Sorry that I have been quit absorbed with "mahangaiko ya maisha haya", here and there to an extent that I have not been participating in many many important topics that have been in our discussions network. I am a bit baffled the way we or most Tanzanians including the entrusted elites look at serious problems ravaging their fellow citizens and remain undisturbed!! I have always lay my blames on leadership on all our problems. This is because they the ones expected to guide, lead and pioneer other community members for any meaningful and fruitful venture. Given right leadership with right policies, poverty becomes just a mental attitude. If a leader is committed to work out with his/her people to solve ant societal problem, the results will just be equal (at minimum) the available resources for the same. We are all aware, that any serious MP in his/her constituency has lived and leave a legacy behind of things he/she accomplished while holding that office.
Therefore Policies and Programs be it on Maternal mortality or children mortality have to yield expected results (o.t.r.e) given the vote owners/mandated leadership care their responsibility of ensuring the plan is implemented to the targeted people and resources provided utilized in time and space. The contributions made here are scientifically correct but is the political will en-culture in feeling the necessity to see the mortality's minimized if not eradicated? Our root problem is leadership lacking commitment morally and ethically hence however good the plans can be, no tangible results as we have lost the art of self regulation and accountability. It is not how much we have but what do we do with the little we have.
Kessy, G. J.
DAR
Martin Mandalu : Tuesday, August 03, 2010
Naam,
kwa hakika kama tulivyoona kuna sababu kadhaa wa kadhaa ambazo zina sababisha vifo vya kina mama wajawazito. Wachangiaji wameongelea huduma dhaifu katika vituo vya afya, zahanati, na hata katika hospitali zetu kubwa. Wengine wameachangia kwenye suala la umbali wa huduma toka kwenye makazi ya wananchi hasa vijijini. Wengine wamechangia suala zima la wito wa uuguzi; kuna madaktari na manesi ambao wana uwezo mkubwa wa kitaaluma lakini wanakosa kujua namna ya kuwa na mawasiliano mazuri na wagonjwa wao. Na kadhalika na kadhalika.
Jambo jingine japokuwa limechangiwa ni suala la vijana wa kike hasa maeneo ya mikoa Pwani kuanza kujihusisha na vitendo vya ngono wangali wadogo. Naam, tatizo hili nimekutana nalo kwa kiasi kikubwa katika wilaya ya Mtwara vijijini.
Wasichana wadogo wenye umri mdogo wa hadi miaka 12 na 13 unakuta tayari wana watoto. Wenye kubahatika kupata watoto ni wachache mno wengi wao hupoteza maisha wakati wa kujifungua.
Tayari kuna elimu inatolewa ili akina mabinti wadogo waendelee kusubiri kushiriki kwenye tendo la ndoa mpaka umri utakapo waruhusu. Kwa kuwa elimu tayari inatolewa basi wadau wengi zaidi wanaofahamu elimu hiyo wajitahidi kujitoa kuwaelimisha jamii hii ya wasichana wenye umri mdogo ili kupunguza idadai ya akina mama wajawazito wanaopoteza maisha wakati wa kujifungua.
Mandalu
Bariki Karosi Kaale : Thursday, July 29, 2010
Waheshimiwa wadau wa TAKNET
Naomba kumpongeza na kumshukuru Dr. Kida kwa nasaha nzuri alizotoa. Vyanzo vya vifo vya dada zetu ni vingi. Ukosefu wa huduma za afya ni moja wapo - kutokana na umasikini.
Naomba kutoa mchango wa awali na baadae nitatoa mchanganua zaidi. (Paper backed by proven research data). .Baadhi ya tafiti zinaonyesha ukosefu wa nishati ya kupikia na mwanga wa taa vinachangia kwa kiasi kikubwa vifo vya wamama ambao ndio wanahusika hasa na kutafuta kuni na kupika kwenye mazingira yenye moshi (in door pollution kitchens). Kwa zaidi ya karne tano asilimia 98 ya Watanzania wameendelea kutegemea kuni kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia. Upatikanaji wa kuni unapungua na sehemu nyingi miti imetoweka. Serikali haina mikakati ya kuhakikisha kuni za kupikia zinapatikana au nishati mbadada (affordable and relaible alternative energy sources for household cooking). Wakina mama wajawazito na wanaonyonyesha wanateseka siku kwa siku kuokuta kuni. Wanatembea zaidi ya km 10 kwa siku huku wakibeba mzigo wa 25-30 kg wa kuni. kila trip kitendo ambacho kinadhoofisha afya zao.
Utafiti unaonyesha kwamba mwaka 1961 kila Mtanzania alikuwa na wastani wa hekta 7.0 za msitu wa asili na kuni zilikuwa nyingi. Kwa mwaka 2009 kila mtanzania alikuwa na wastani wa 0.7ha za msitu wa asili na kuni zinapatikana kwa shida. . Kwenye maeneo mengi hapa nchini miti mikubwa imetoweka kwa hiyo ardhini hakuna tena mbegu za miti ya asili tuliyozoea ambayo inatoweka kwa kasi kwani haitaweza kuota tena kutokana na ukosefu wa mbegu...
Kuni/mkaa zinachangia asilimia 92 ya nishati inayotumika Tanzania bali ni chini ya asilima 0.3 ya bajeti ya nishati inatumika kuendeleza upatikanaji wa kuni.. Kipau mbele cha maendeleo ya nishati ni umeme ambao hadi sasa ni chini ya Watanzania 600,000 kati ya 42,000,000 wanatumia umeme kwa kupikia. Umeme umepewa zaidi ya asilimia 99.6 ya bajeti ya nishati mwaka huu wa fedha. Pamoja na hizo juhudi nzuri - tatizo lililopo ni kwamba Watanzania walio wengi hawataweza kupikia umeme kwa siku za karibuni. kwa hiyo wataendele kutegemea kuni/mkaa.
Kutoweka kwa misitu kutokana na kuni - ambazo ni hitaji muhima la kila siku kwa maendeleo ya kaya pia kunachangia uharibifu wa mazingira, hasa uharibifu wa vyanzo vya maji na kufanya maisha ya wakina mama kuwa magumu zaidi.
Kwa maoni yangu juhudi za pamoja zinatakiwa kufanywa na kila sekta kutatua tatizo lililopo. Sekta ya afya ni sehemu tu ya wadau na tunawashukuru kwa mchango wao. Sekta zingine kama nishati, viwanda, elimu, hazina n.k ziwepo. Bariki K. Kaale ( Mtaalamu wa Nishati UNDP -TZ)
japjet Makongo : Wednesday, July 28, 2010
Tafiti zimetuonyonyesha kuwa baadhi ya sababu za vifo vya mama wajawazito vinatokana na ukatili wa kijinsia hususani majumbani. Wanawake wanapigwa, kunyanyaswa na kusababishiwa ulemavu wa kudumu na hata kuathirika kisaikolojia. Njia ianyotumika ni kuwalemisha na kuwawashawishi wanaume washirki kikamilifu katika malezi ya ujauzito wa akina mama, ikiwa ni pamoja na kuongozana nao katika vipindi vya kiliniki.
Inawezekana kuna badhi ya wanaume walioanza kuhudhuria klinik na wake zao au wapenzi wao japo kwa kasi ndogo. Kwa sasa ni vigumu kuwajua kwa vile hakuna mfuo unaochukua rekodi zao katika kliniki na vituo vya afya. Kinachotakiwa ni kurekebisha daftari za rekodi za MTUHA ili kuwepo na sehemu ya kujua wamaume wangapi walihudhuria na wapi. Inawekezekan hii ikaonekana kuwa sababu ndogo, lakini nadhani itejenga kivutio kwa wanaume. kazi kwenu wizara ya afya.
Makongo
Omari Mwinyi Khamis : Monday, July 26, 2010
I completely agree with Irene Alenga that men can play a big part in this problem.That theheath care program that takes place at theNgaranaro Health Centre in Arusha should actually include men as well. Husbands should follow their wifes in such a training.I remember to follow my wife to th hospital in Sweden when she was pregnant and we were both trained as how to act in different situations.I was also present during the last moment during the birth of the children.
However, there are some complications that require the experience of a nurse or a doctor.Therefore pregnant women have to be advised to visit hospitals ferequently if they detect something is wrong.The medical information is of paramount importance in several pregmant cases and can save serevral lives.
Yes Dr.Tausi Kida there is no nation without people and our politicinans knows this very well.We need to incerse the health budget from 7.74 USD to at least 10.5 USD per year.We must take care of the future generation not only in education but also in health maters.
Dr.Khamis
Dr. Tausi Kida (Moderator) : Thursday, July 22, 2010
Dear TAKNET members
Napenda kuwashukuru kwa maoni yenu mliyoyatoa mpaka sasa kuhusu tatizo hili la vifo vya akina mama kutokana na matatizo ya ujauzito. Kwa kweli tatizo hili ni kubwa kote mijini na vijiji , lakini takwimu zinaonyesha kwambasehemu nyingine kijiografia zimeadhirika zaidi ya nyingine na hasa sehemu za vijijini. Baadhi ya takwimu kuhusiana na suala hili zinaweza kupatikana katika ripoti ya PHDR 2005, ambakomaternal mortality rates (MMR) zimeripotiwa katika ngazi ya wilaya.
Katika kutafuta ufumbuzi wa suala hili ( kama baadhi ya wadau walivyosema) kunahitajika kufanyika utafitiwa kina ili kufahamu kiini cha tatizo na pia kuhusisha matatizo mengine nje ya sekta ya afya( other structural problems) yanayochangia kuongezeka kwa tatizo hili mfanongazi ya elimu kwa jamii, mila potofu etc.
Ni vizuri kuzingatia kwamba ufumbuzi wa tatizo hili utahitaji hatua za haraka (immediate measures) zikihusishwa na mipango ya muda mrefu.Serikali pia inatakiwa kuwa na wito madhubuti hasa katika kutenga fedha kwaajili ya kuboresha huduma za uzazi . Ni muhimu kujua kwamba kwa sasa nchini Tanzania ni asilimia 15 tu yazahanati zina uwezo kutoa huduma bora kwa masaa 24 kwa mama wajawazito. Hivyo basi jitihada zinahitajiwa kuboresha vitendea kazi katika kutoa huduma hii i.e improvement of infrastructure for obstetric care.Hivyo hakunabudi kuongeza matumizi ya fedha katika kuboresha huduma hii na kupunguza matumizi mengine yasio na lazima . Je tuko tayari?Ikizingatiwa kwamba allocation ya pesa za afya kwenda katika ngazi za wilaya imekua ikiongezeka kwa asilimia ndogo sana ( angalia PER 2008). Pia our per capita health spending bado ni ndogo sana 7.74 (USD) - bajeti ya asilimia 7.74 kwa mtu kwa mwaka – katika mwaka 2007/2008 ukilinganisha na target ya WHO ya USD 34 kwa mtu kwa mwaka.
Pia suala zima la kutoa huduma bure kwa akina mama wajawazito linatakiwa liangaliwe kwa kina na lisibakie katika sera tu.Wakina mama wengi bado wanahangaika kutafuta fedha za vifaa muhimu kama clovesna nyuzi, kulipia huduma za usafiri na chakula pindi wako hospitali , na pia kuwa na fedha za kutoa asante kwa wakunga n.k. Hali hii inaleta utatanishi mkubwa kwa wakina mama wakati wanapokwenda kujifungua
Regards,
Mwisomba Titus : Thursday, July 22, 2010
Ndugu Wa TAKNET,
Naitwa Likanga, nimejiunga jana tu na Mtandao huu na ni imani yangu kuwa wengine wataendelea kuja kwani ni mahali pazuri kwa kupashana habari.
Kwa maono yangu ninafikiri hili tatizo la Vifo vya akina mama kutokana na matatizo ya Ujauzito, linaweza kutatuliwa na wadau wote kwa ujumla, yaani Serikali, NGOs, Wanakaya wenyewe kwa kushirikiana na kuliona kuwa hili ni tatizo. Inawezekana kabisa kama juhudi za kujenga hospitali na kuboresha huduma za afya zikifanywa kwa pamoja (Participatory Approach), tatizo hili linaweza kuwa ni hadithi za kale.
Pia Elimu itolewe kwa wote (Baba, mama na wanafamilia) juu ya umuhimu wa kujifungulia Vituo vya Afya. Akina mama wengine hawawezi kujifungua katika kituo cha Afya kwa sababu Mkunga aliyekuwepo pale ana umri sawa na Mwanae wa kwanza, hivyo anaona heri ajifungulie nyumbani chini ya Mkunga wa jadi ambaye hata hivyo hajapata mafunzo. Kwa hiyo hapa ni swala la "change of mind set". Hivyo ni muhimu elimu shirikishi ikatolewa na Wizara husika kwa kushirikiana na wadau wengine.
Kuwe na mawasiliano ya mara kwa mara kati ya Wakunga wa jadi pamoja na watoa huduma ya afya chini ya Wizara ya Afya, ili kupata mjulisho nyuma wa kile kinachoendelea katika Jamii. Kwa upande wa Serikali ihakikishe inasimamia vyema huduma hizo, isiwe kwamba sheria ipo ya akina mama wajawazito kupata huduma bure kutoka katika vituo vy afya, lakini sheria hiyo haitekelezwi na wale waliopata majukumu ya kuyasimamia. Kwa mfano, gari la wagonjwa lipo, ila ukifika na mama mjamzito unaambiwa gari halina mafuta, hivyo uchangie. Sasa hiyo inaweza kuwa ni tatizo kwa wengi kwani kiasi hicho wanachoambiwa kinaweza kuwa kipo nje ya uwezo wao.
Wapendwa, mimi nimeliona tatizo hilo kwa jicho hilo, lakini bado mwingine anaweza kuliangalia kwa jicho lingine pia.
Asante
Likanga
Omari Mwinyi Khamis : Thursday, July 22, 2010
Swala la vifo vya mama maja wazito ni ngumu sana hata kwa chi amazo zimeendelea.Mfano wa mja mzito kucheleweshwa kwa sababu hakuna gloves ni kwa sababu ya kinga yake ili asipate magonjwa kama AIDS wakati wa uzazi.
Jambo muhimu kwa nchi nzima ni kupanua huduma za waja wazito ili waewe kupewa upelelzi wa mimba zao mara kwa mara pamoja na matibabu yanayo hitajika.Mama waja wazito hawatakiwi kufanya kazi za dharubu.Kwa mfano nilpokuwa nafanya kazi katika mgodi Sweden tulikuwa na mwanamke ambaye alikuwa anafanaya kazi ya kuchimba mgodini.Lakini alipokuwa na miba ilibidi tumpe kazi nyingine ambayo haihitaji kutumia nguvu.Tulimpa kazi ya kuchora ramani za mgodi(production unit).
Pia wajazazito wanahitaji kuelimishwa na kufanyiwa uchunguzi mara kwa kwa mara kati ya mwezi wa sita na nane mpaka mwezi wa tisa.Mama wakunga ndio ambao wanayo elimu hii ya kuwasaidia majawazito.Wao wangeliweza kutambaza elimu kwa jamii kwa kutumia vyombao vyote vya harari nchini.
Der.Khamis
Sweden
Bughali Frank : Thursday, July 22, 2010
It is true that maternal motarity is realy a problem in most of all african countries.the cause of this problem is that there is abig gap between health workers and women, so if we creat friendship between this two sides it will reduce the problem.this is because many women fears the abusive laguage used by nurses
IRENE ALENGA : Thursday, July 22, 2010
I will start my contribution with a preamble. Following reserch that has been done by the UNFPA world wide, maternal and child mortality rates are a big indicator of poverty in any country in the world. Maternal mortality is the largest health inequity in the world; 99 per cent of maternal deaths occur in developing countries – half of them in Africa. A woman in Niger faces a 1 in 7 chance during her lifetime of dying of pregnancy–related causes, while a woman in Sweden has 1 chance in 17,400. With a record of 529 maternal deaths in every 100,000 women in a population of almost 40 million people where does this place Tanzania? Have we not been able to save the lives of our mothers, sisters, daughters, wives because of poverty?
We have all discussed about government interventions but what is our role as individuals? At a nuclear level, what is the husband’s/ faters role in ensuring the safety of the expectant mother? I read with a lot if interest an article in the Daily news published on the 21st July 2010 on how husbands can reduce maternal deaths. If we digress into this perspective they play a very major role to the well being of the expectant mother from conception to delivery and post delivery periods either physically, mentally, spiritually or emotionally. This person spends a susbtatial amout of time with the pregnant woman and would therefore be able to track the development of the pregnancy and be the first engagement point if any complications develop. So while a lot of efforts have been focussed on the women we should not ignore the men. This should be the best point of intervention.
We should specifically target this group of individuals and engage them in pre-natal care training. In western cultures, the responsibility of parenthood is a shared one unlike African culture where there is a clear division of labor for men, women and children where roles are properly defined and strictly followed. I talk in this perspective because most of these deaths are experiencd in rural areas. True to experience given by most of the contributors, access to facilities, properly trained doctors, nurses and midwives or even equipment contribute to these deaths but lets not forget knowledge is power and that’s why we have advocate for First Aid to save lives. It is the first response to any complication in expectant mothers that hangs their balance for survival.
At the Ngaranaro Health Centre in Arusha, there is a training program offered every morning to pregnant women called the “Individual Birth Plan Training” Imagine what a differene it would make if husbands/ fathers also attended this training alongside their partners.
Festo E. Maro : Wednesday, July 21, 2010
Ningependa kwenda moja kwa moja kwenye mchango wangu kuhusu hii mada kwani waliotangualia wamesha elezea umuhimu na kuiweka mada hii katika mtazamo wa majadiliano. Ni jana tu usiku nilikuwa nasilikiza na kutizama TBC1 ambapo reporter wa Mkoa wa Songea alikuwa anaelezea adha ambazo mama wajawazito wanaendelea kuzipata hata baada ya miaka arobaini ya uhuru. Katika taarifa yake nimeona kuwa uhuru huu ni kwa wengine lakini siyo mwanamke ambaye ni mjamzito. katika hiyo taarifa nilisikia kwenye hiyo hospitali ya mkoa wa ruvuma vipo vitanda 50 tuu katika wodi ya wazazi lakini huwa kuna mama wajawazito walio jufungua na wanaotaka kujifungua kati ya 80 na 100. Daktari alisema inabidi kitanda kimoja kitumiwe na wajawazito wawili mpaka watatu. Hali hii inasababisha kila mama mjamzito aje na msaidizi wake kutoka nyumbani ambaye atalala nae kuangalia mtoto asije kulaliwa au kudondoka chini. Manesi waliopo hawawezi kuwaangalia wajawazito wote kwa ufanisi. Ukitafakari hali hiyo katika za wodi za wajawazito utaona kuwa msongamano nimkubwa sana. Hali hii ina sababisha matatizo mengine kama hali ya hewa kuwa nzito kusababisha watoto wachanga na mama wajawazito kupumua kwa taabu. vilevile utaona kutakuwa na msongamani mkubwa katika matumizi ya huduma zingine kama vyoo na mabafu. Daktari wa hiyo hospitali alisema hiyo imekuwepo hapo hospitalini kwa mda mrefu sana na kwa mda wa miaka miwili amekuwa anafuatilia kwa karibu bila mafanikio ya haraka. Maranyingi viongozi huwa wanajitetea kwa kusema fedha hazipo kukidhi mahitaji ya kuboresha wodi za wajawazito. Lakini chakushangaza wabunge walidai nyongeza za mishahara yao bila hatakufikiria kiasi hicho cha fedha kingeweza kuleta tofauti katika sehemu mbalimbali hapa nchini. Kuna haja ya kuweka vipaumbele kwenye maeneo ambayo ni muhimu hasa miundombinu ya kuwahudumia mama wajawazito ili kupunguza vifo na taabu wanazozipata.
Angomwile Fungo : Tuesday, July 20, 2010
Tatizo linaweza kuwa kubwa kuliko vile linavofikiriwa, kwa sababu kuna wale walioko vijiji vya ndani ndani kama Lendikinya(Monduli) ambako upatikanaji wa data ni karibu na hamna.
Sababu ya Vifo,
Kuchelewa kufika hospitalini/dispensary.
Mimba katika Umri mdogo.
kwa wale wanao wahi hospitalini, uzembe wa wakunga(hasa hospitali za serikali).
ukosefu wa elimu ya uzazi (hasa vijiji vya ndani ndani na kiasi mijini) kwa wakunga na wazazi watarajiwa pia.
Napendekeza,
Uzembe wa Wakunga. Apo ndio kuna balaa kama nini. SULUHISHO, linahitaji mipango ya kudumu na muda mrefu_kuelimisha wakunga kuhusu umuhimu wa kazi yao kwa jamii, kuboresha maslahi yao, na kuelimisha jamii kuhusu haki zao za kiafya. Uwepo usimamizi (kama vile audit ivi). na kuwaondoa wale wanaobaininka kuzembea.
Kwanza kuwe na utashi wa kisiasa, kiuchumi, na kijamii tokea chini. yaani kuanzia na wazazi watarajiwa wenyewe, wanasiasa na watendaji serikalini. hii inasaisia kuleta PRESHA ya mabadiliko ya lazima kama kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya mambo ya uzazi kuanzia na familia mpaka serekelini.
Miundo mbinu iboreshwe
Jamii hususani wazazi watarajiwa wale vijana wanaotoka utotoni kwenda utu uzima wapate elimu ya kutosha kuepusha mimba katika umri mdogo. elimu hii itolewe mashuleni, misikitini, makanisani yaani mahali popote ambapo watu wenye nia moja hukusanyika mara kwa mara.
elimu ya ukunga wa jadi iendelezwe na kuboreshwa.
Grace Millinga : Tuesday, July 20, 2010
Napenda kuanza kwa kuwashukuru taknet kwa mada nzuri mliyotoa. Kwanza napenda kumuunga mkono Mr.Adolph Massawe, Kwa kweli this is a big problem kwetu Tanzania and other developing nations,linaumiza na linamaliza ndugu zetu ambao ni wajawazito na hasa hawa vichanga ambao hupoteza maisha either kwa huduma mbovu aipatayo mama au kutokuwepo kwa huduma za afya karibu. Mimi kwa upande wangu nahisi ufumbuzi wa tatizo hili ni kuhakikisha huduma za mama wajawazito zinaboreshwa ikiwa ni pamoja na madawa,vifaa,usafi na uangalizi wa karibu wanapokuwa wodini.Nasema hivi kwasababu ni siku nne tu zimepita tangu dada yangu ajifungue na nilipokuwa hospitali nilishuhudia mama mjamzito alicheleweshwa kupewa huduma eti kwasababu hakukuwa na gloves.
david masambe sando : Tuesday, July 20, 2010
Napenda kutoa maoni yangu pia katika hili kwani limenigusa pia !
Ni kweli kabisa, ukiwa kwenye huduma ya tiba utagundua hospitali zina asilimia fulani kwenye kuchangia haya, hata hivyo mambo mengi yanachangia tena kwa aslimia kubwa,
Ni mambo mengi sana ikianzia elimu ya mzazi, miundombinu ya kumpeleka mama hospitali, uwepo wa karibu wa vituo vya afya na mengine mengi. Kwa ukweli vifo vya akina mama vinavyotokea mahospitalini mara nyingi ni mama kufika akiwa amecheleweshwa na yuko katika hatua mbaya sana, ingawa sisemi kwamba kuna ambavyo wahudumu wanachangia na mazingira ya kazi.
So vifo vingi ni michango ya mambo mengi ambayo hata ukiwa na hospitali kote nchini na karibu na wananchi, kama maendeleo bado chini na elimu ni duni havitaisha, tatizo nimfumo mzima wa maisha na huduma za jamii
Tuangalie kwa mapana zaidi
regards
Kamala Lutatinisibwa : Tuesday, July 20, 2010
Nacnhangia hapa nikiwa nimetoka kupata mtoto siku mbili zilizopita. niliilazimika kuachana na hospitali ya mkoa wa Bukoba kwa uuzoefu wa waliotangulia kupaa huduma pale na hivyo kulazimika kumpeleka mke wangu hosp ya misheni na ya wilaya ya missenyi ili kuapata huduma, sikuamini kuwa niliambia napaswa kulipia shs 1,500 tu kwa siku zote mke wangu alipokaa pale lakini pia huduma zilikuwa nzuri. japo mimi sio mpenzi wa siasa lakini nafikiri hii nihatua kuubwa ya kuokoa maisha ya wazazi na watoto.
Ila changamoto zilizobaki ni kama vile usafiri wa kupelekwa hao wakazi wa vijijini hosp. kwa mkoa kama kagera wamejitahidi kwamba bara bara zoote zinapita kwa kiasi. ila sasa umasikini wa wazazi kupata usafiri wa kuwawaisha inabidi uangaliwe upya
Tunahitaji juhudi za makusudi, kwa mfano kuwezesha wazazi kuishi karibu na hosp au karibu na usafiri waonapo siku zimekaribia. kuajaribu kujitengea pesa waonapo siku zimekaribia na kuka makini muda wote
EUSEBIO J. CHILIPWELI : Tuesday, July 20, 2010
Mimi mchango wangu ni mdogo tu. Ningependa kwanza tatizo hili kwa jinsi lilivyo liainishwe kwa misingi ifuatatyo na ndipo tuanze kutatfuta njia za kulikabili:
1. Jinsi tatizo lilivyo kwa wakazi waliopo mijini ambako huduma zipo karibu, ni kiasi gani au kwa kiwango gani tatizo hili lipo!
2. Kwa kiwango gani tatizo hili lipo vijijini ambako diko waliko akina mama wengi walio mbali na huduma za afya.
3. Mila na desturi zinachangia kwa kisai gani kubaki au kukua kwa tatizo hili, na ni maeneo yapi yenye kugubikwa zaidi na tatizohilo na kuhitaji msukumo wa pekee katika kulikabili.
4 Kutokuruhusu tatizo hili liedeshwe kisiasa badala ya kutumia takwimu na hatua madhubuti kulikabili.
Kwa maoni yangu swala hili limo midomoni mwa wanasiasa wetu kila wanapotafuta umaarufu kwa wapiga kura wakati wanapowahitaji wawape "ulaji". Wakisha pata ulaji hawana tena nafasi ya kuangalia yanayowasibu waliowapa ulaji, hasa akina mama ambao ni ndio wapiga kura wengi.
Ni muhimu kuainisha ni vitu gani vinavyoletea 'maternal motality'
katika mazingira yapi ( mijini na vijijini) ndipo tuone jinsi gani tunaweza kukabiliana navyo. Nani afanye kazi hiyo?
Labda niachie mchango wangu kwa sasa hapa ili wenzangu tupate nafasi ya kuuendeleza.
E.Chilipweli.
Gideon Karuguru : Tuesday, July 20, 2010
Naomba nijitambulishe kwa wan TAKNET kwamba mimi ni mdau mpya naitwa Gideon Mabanga Karuguru.
Awali ya yote napenda kuungana na wachangiaji waliotangulia na pia kuwapongeza kwa michango yao. Kutokana na uchangiaji huu tunapata picha kwamba tunao watu, wanaoelewa na kuugua kutokana na utendaji mgando ulioko katika mfumo wetu na serikali, baadhi yetu tukiwa humo humo ndani na pengine kutokana na mazingira yaliyopo tumeshindwa kufanya mabadiliko.
Niungane na Apronius Vitalis Mbilinyi katika baadhi ya vipengele kwa kuchangia ifuatavyo:
Suala la vifo vya akina mama kutokana na matatizo ya ujauzito (Maternal Mortality) huwezi kulizungumza kwa kulitenga na vifo vya watoto wachanga (Infant Mortality) na hivyo linachukua sura pana zaidi ya namna linavyoonekana. Changamoto kubwa inayotukabili sisi kama nchi inatokana na namna tunavyofikiri, kupanga na aina ya watu ambao tumewapa dhamana ya kutengeneza mipango yenyewe na kuweko kwa siasa zisizo halisia.
Nianzie na suala la watumishi: kwa wakati tuliomo Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inatekeleza Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) na ndiyo msingi mkubwa wa 'sera' ya zahanati kila kijiji na kituo cha afya kila kata. Binafsi si muumini wa 'sera' hii kwa sababu naamini katika kuchapa kazi kwa bidii, uaminifu na umakini ili kupata matokeo yaliyo bora. Naomba nikariri msemo kutoka gazeti la Majira J3, kwamba 'maisha bora hayawezi kuja kwa kucheza pool'. Ni kama vile tunacheza pool, tunachezea pesa, tunapoteza mchezo mmoja baada ya mwingine wakati huo huo tukiota kujenga nyumba na kuishi maisha mazuri ilhali kazi hatufanyi. Naomba nirudi kwenye mada.
Mojawapo ya malengo makuu katika MMAM ilikuwa ni kuzalisha wataalam wa kutosha ili waingizwe katika ajira ya umma na kusaidia kuboresha ubora wa huduma inayotolewa na zahanati na vituo vya afya. Batch ya kwanza ya wataalam wa kada za utabibu na uuguzi kwa ngazi ya cheti imetoka mwaka jana mwishoni na mwaka huu mwanzoni, wengi hawajaajiriwa kwa sababu hakuna vibali vya ajira kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi, kwa sababu Hazina haikuwa na pesa ya kutosha kwa ajili ya mishahara, kwa sababu mapato ya Serikali na hasa makusanyo ya kodi kutoka TRA yameshuka na pesa haitoshi, kwa sababu watu wengi hatulipi au tunakwepa kulipa kodi, kwa sababu ...... wenzangu mwaweza kuendelea kunyumbulisha.
Ukiacha wataalam hawa wa kada za chini ambao hawajapata ajira, tuangalie ajira ya madaktari wanaofuzu kutoka vyuo vyetu vikuu, kwa sasa tunazalisha takribani madaktari 600 kwa mwaka (mwenye takwimu nzuri atanisahihisha) lakini kwenye ajira ya umma wanaingia wastani wa 200 kwa mwaka, wanaobaki wanatafuta pa kwenda, baada ya kuwa tumewapa grant ya kusomea taaluma hii muhimu, wanachukuliwa na wengine. Je, tuna nia makini kweli ya kupunguza matatizo yetu?
Ukiwasikiliza waheshimiwa wanazungumza wanakiri kwamba huduma zetu za afya zinatolewa na watu wenye utaalam wasiozidi 40%, maana yake tuna pengo la 60% kufikia viwango vya kimataifa, kama ndivyo, je tunahitaji vibali kuajili wataalam tuliowaandaa sisi wenyewe kwa gharama zetu na wakati huo huo tukitambua kwamba kuna wataalam wanastaafu na kufa kila siku inayopita? Je tunahitaji kweli kuongeza majengo ya zahanati na vituo vya afya wakati vilivyopo havina wataalam? Tunahitaji zaidi maamuzi na kuwa wa kweli.
jason nkyabonaki : Tuesday, July 20, 2010
Napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza kwa kuamsha mawazo namna ya kuzuia vifo vinavyotokana na uzazi.Mimi najielekeza kwenye nadharia ya kiutamaduni(cultural relativism theory).Dhana kubwa hapa ni kwamba kabla ya hospitali hizi tulizonazo leo,tulikuwa na mfumo wa tiba za asili na ambazo zilifanya kazi vizuri.Wanawake wajawazito walikatazwa vyakula fulani fulani kama mayai wakiambiwa mtoto angezaliwa bila nywele,nakadhalika. Pili,tulikuwa na dawa za kiasili ambazo wakunga wa jadi waliweza kutoa na akina mama wakaweza kunywa na kujifungua salama.Leo hii,ni mama yupi atakubari kunywa hizi dawa kama si kwenda hospitali na ambazo zimesongwa na matatizo mbalimbali lakini pia ambazo zinaweza zisitusaidie kwa maana kama kule Kagera watu husema kuna magonjwa ya kwenye kitovu(inherited diseases)ambayo hata hospitali wanaweza wasiwe na dawa lakini wao hujua historia ya ukoo katika mfumo wa uzazi.
Kutokana na mawazo hayo mimi nahisi suluhisho tufikirie upya tiba yetu ya asili na hii ndo motto tunaoita(African Renaissance).Hivyo basi turudi na sisi wenyewe tuboreshe kiwango cha tiba zetu za asili kwa kuwatumia bibi zetu kupata tiba ya asili. Tukumbuke hatutapoteza tena maisha kama tukirudia kile ambacho tumekipoteza kwa kuambiwa ni kibaya au ni uchawi ili huyo mtu atumie mti huohuo aukaushe na akwambie usafiri kilometa 1000 kufuata mahali panapoitwa hospitali badala ya kufuata kwa mama Koku ambaye yuko mita 100 tu.
Nafikiri tujielimishe na tubadili attitude zetu kwa kile Thiongo anachoita "Decolonization of the mind" tukifanya hivyo tutapiga hatua na vifo vitokanavyo na uzazi itakuwa historia na tunaweza kuwa msaada mkubwa kwa taifa na bara zima la Afrika.
Apronius Vitalis Mbilinyi : Monday, July 19, 2010
WanaTAKINET wenzangu. napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wasimamizi wa mtandao huu kwa kuleta maada hii. Vifo vya akina Mama kutokana na ujauzito ni tatizo ambalo linasikitisha na kutia aibu kwa nchi yetu kwani ni imani yangu kwamba kama watanzania na serikali yetu tukijipanga vizuri tunaweza kupunguza zaidi ya nusu ya vifo hivi nahivyo kwenda sambamba na malengo ya Milenia na MKUKUTA.
Ukiangalia takwimu za wizara zinasikitisha kwani kila siku moja zaidi ya mwanamke mmoja hufa kwa tataizo linalotokana uzazi Kwa maoni yangu ni sababu ya kuendelea kusumbuliwa na tatizo hili ni kwamba kama ilivyo matatizo mengi ambayo hatujajipanga vizuri na hivyo yanaendelea kutusumbua. Nadhani serikali inahitaji kuwa na mipango ya muda mfupi na mrefu katika kutatua tatizo hili (kwa taarifa mipango hii ipo), sasa tatizo lipo wapi?. Ukichunguza sana utajua tatizo ni lile lile kama ilivyo kwa utekelezaji wa matatizo mengine kama kuondoa tatizo la ukosefu wa elimu, nishati, maji, barabara...nk.
Watanzania tuna ugonjwa wa kuzungumza sana na kutenda kidogo sana na wazuri wa kujitetea kwa nini hatukufanikiwa. Tukibadilika tuta tatua tatizo hili. Ushauri wangu ni kwamba tutekeleze mipango tuliyojipangia.
Mipango ya muda mfupi tunayoweza kutekeleza ni kama kutoa elimu kwa wananchi wote(hasa wanaume) kupitia vyombo mbalimbali vya habari kuwa kina mama watajifungua salama zaidi hospitali (dispensari) kuliko majumbani, pia tuendelee na kufundisha wakunga wa jadi wengi zaidi. na mipango ya muda mrefu iwe kama kuwaandaa watalaamu wengi bila kufikilia sana faida ya muda mfupi, kutoa vivutio kwa vijana wanaotaka kusomea fani ya udaktari , kufanya kampeni kwenye mashule ili kuwashawishi vijana wengi kusoma masomo ya sayansi ili kupata wataalamu wengi siku za baadae, kuwalipa vizuri wataalamu wa afya ili kuwabakiza hapa nchini (avoid brain drain), Kuanda vivutio kwa wataalamu kufanya kazi vijijini. na pia kuendeleza mpango ulioanza wa kuwa na zahanati kila kata au kijiji.
Hata hivyo Kuondoa tatizo hili kunahitaji utashi wa siasa pia (political commitment) kwani tutahitaji kutenga fedha za kutosha kwa sekta ya afya na mhimu ni kuhakikisha kwamba fedha hizi zinafika hadi ngazi za chini na kutumika ipasavyo.
Dorah Semkwiji : Monday, July 19, 2010
Aksante sana TakNet kwa kutupatia tena nafasi hii ya kuchambua mada mbalimbali zinazoelezea mustakabali wa watanzania. Napenda kushukuru kwa mada hii ya vifo vya akina mama na ongezeko lake kila kukicha licha ya jitihada zinazoonekana kufanywa.
Ninaungana kabisa na wachangiaji waliotangulia. Kusema ukweli ninapolifikiria hili suala mimi huwa kidogo naona kama bado jitihada za lazima au tuseme msisitizo wa lazima katika kutatua tatizo hili hazijafanywa kikamilifu. Nina imani kabisa na serikali yetu kuwa ikiamua kushughulikia jambo inaweza kabisa tatizo tu ni wapi tunapoweka priorities zetu. Tukiangalia priorities zinazowekwa katika nchi yetu kwa kweli nyingi huwa zinalenga katika kuukuza uchumi wa nchi yetu. Najua kuna watakaosema kuwa uchumi wa taifa ukikua basi na huduma nyingine zitaboreka ni kweli lakini tusisahau pia umuhimu wa ugawanywaji ulio sawa wa hayo maendeleo kwa sababu nchi inawezakuwa na uchumi mkubwa lakini ukamilikiwa na wachache -huku ukiwaacha wengi wakiwa na hali duni kiasi cha kuwafanya wakose huduma muhimu za maisha. The same applies katika level ya kitaifa kuwa tunawezakuwa na uchumi uliokuwa lakini ukaishia katika kuboresha sehemu tu ya huduma za jamii mf. elimu na kuzisahau nyingine au hata kutoa uwiano usio sawa.
Nikiiangalia hali ya huduma za kina mama ninajiwa na mashaka kana tutawezakutimiza lile lengo la milenia juu ya kupunguza vifo vya akina mama wajawazito. Nafikiri serikali yetu inatakiwa itilie mkazo sana juu ya hili na pia iwepo sheria ya kuadhibu wauguzi wazembe ambao kwa namna moja au nyingine huchangia sana katika vifo hivi. Ni mara nyingi tumesikia vifo vya kizembe na kuishia kusema ni bahati mbaya au siku yake imefika ilhali aliyesababisha uzembe anabaki akichukulia kuwa ni busness as usual kiasi kwamba hata kesho akifanya mwingine ataona sawa tu bila kujali kuwa maisha ya binadamu yakipotea hakuna cha kufidia kwa familia iliyopotelewa.
cecilia valla : Monday, July 19, 2010
Nakuunga mkono Khalfan- na iwapo TOR ita tengenezwa, tunaweza kuona vile tuta saidiana kutatua MMR yenye iko juu sana Tanzania- currently 558.
If anyone has any documents to show the high MMR in various parts of Tanzania tafdhali please send to me. cecilia.valla@worldvision.com.au
Thanks,
Adolph massaswe : Monday, July 19, 2010
Asante kwa swala la msingi la vifo vya wanawake wajawazito. Napenda kutoa mchango wangu hapa naona yafuatayo yawekwe wazi kwa watanzania: 1. Watu waelimishwe vya kutosha kuhusu mimba za utotoni 2. Wakinamama waelimishwe (kiliniki) wakiwa wajawazito waelewe undani na dalili mbaya zinazoweza kutokea 3. Serikali itoe huduma za karibu za kijamii mfano hospitali ziwe karibu na makazi ya watu 4. Pia kuhakikisha kuwa usafiri ni bora ukizingatia barabara ili mamamjamzito aweze kufika hosp mapema 5. Kuwapa moyo hata wakunga wa jadi ambao hutoa huduma ya kwanza kwa maeneo yasiyokuwa na hospital karibu Nafikiri tukiangalia hilo swala kwamtazamohuo tunaweza kupata na mawazo mengi mapya yatakayotusaidia asanten
Khalfan Salim Suleiman : Monday, July 19, 2010
to me nahisi hii ni jambo zuri sana kujadili lkn katika jitihada za kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili kwanza ni vyema tukaka chnini na kuangali tatizo liko wapi na linasababishwa na nn ili tupate kuja kiini cha matatizo hivyo basi we need to carry out /conduct need assessment of maternal mortality this will produce various informatyion with base line subsequently will result into developing sort of strategic plan withj operational plan that inlcude strategic objectives for fighting against maternal mortality.
tukiweza kuona wapi tunamapungufu ndio tunaweza kupanga mpango madhubuti na makakati kwa kupambana na suala hili ili tuweze kufikia lengo kwani mm nahisi niwaombe saaana wataalamu wa afaya kushirikiana na wataalamu wengieo yaan other stakeholders to kuundertake assessment ya issue hii na baadae ku come up with action plan and finaly to develop strategic document for fighiting against marternal mortality.
Hivyo Muhimbili andaeni ToR for the assessment in order the stakeholders and other intersted persons to participate for kwa hivyo natoa wito kwa umma tusaidiane kenwye hili ili tuwe na focus na sio tuende to bila na pakuanzia na vil vile tuwashajiishe Donors countries to support the effort hata hivyo kila mdau wa hili atengezewe uwajibikaji wake.
Wizara ya Afya awajibika kivyake na wengineo ili tupate collective effot
Dr. Tausi Kida (Moderator) : Friday, July 16, 2010
Wapendwa TAKNET members,
Tunapenda kuchukua nafasi hii kuwakaribisha tena wote kutoa maoni yenu kuhusu mada hii mpya VIFO VYA AKINA MAMA KUTOKANA NA MATATIZO YA UJAUZITO (MATERNAL MOTALITY) NI TATIZO KUBWA TANZANIA. NINI KIFANYIKE KUTATUA TATIZO HILI?
Madhumuni makubwa ni kupata maoni yenu kuhusu jinsi ambavyo serikali na wadau wengine wanavyoweza kusaidia kuondoa hili tatizo. Ukizingatia kwamba kati ya wanawake 100,000 wanawake 578 wanafariki duniakutokana na matatizo ya ujauzito (THDS 2004) . Mbaya zaidi pamoja na jitihada zote zinazofanywa na serikali na wadau wengine tatizo hili limekuwa likiongezeka badala ya kupungua.
Maoni yenu ni ya muhimu sana katika kupatia ufumbuzi wa haraka tatizo hili ; kwa maelezo zaidi tafadhali soma utangulizi hapo juu
Karibuni sana, Moderator: Dr Tausi Kidana Dr Riziki Ponsiano